MIMI SIO RAISI
MAKAMU wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad amesema kupanda kwa bei za bidhaa kutoka kwa wanaozalisha pamoja na kuongezeka kwa gharama za usafirishaji kunakotokana na tishio la maharamia katika ukanda wa bahari ya Hindi, ndiko kulikopelekea kupanda kwa bei za bidhaa nchini, ikiwemo mchele.
Makamu wa Rais, ambae pia ni Katibu Mkuu wa CUF Taifa, ametoa ufafanuzi huo jana alipofungua Mkutano mkuu wa mwaka wa Chama hicho Wilaya ya Mjini, katika ukumbi wa Jamat Khan Mjini Unguja.
Amesema Dunia, ikiwemo nchi wazalishaji wa chakula zinakabiliwa na majanga mbali mbalii yanayopelekea kupungua kwa kiwango cha uzalishajili, huku gharama za usafirishaji zikiongezeka kutokana na vitendo vya uharamia vinavyofanywa na jamii ya Wasomali katika ukanda wa bahari ya Hindi.
Maalim Seif amelazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya kuibuka hoja na malalamiko mbali mbali kutoka kwa wanachama wa Chama hicho dhidi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo katika mfumo wa Umoja wa Kitaifa, wakiuhusisha moja kwa moja na upandaji wa gharama za maisha pamoja na kuwalaumu viongozi wa CUF, akiwemo yeye kwa kukaa kimya hata pale wanapokumbwa na kero zinazohitaji msaada wao.
Alisema wakati Serikali ya awamu ya saba ikiingia madarakani bei ya mchele katika soko la dunia ilikuwa dola 530 kwa tani, lakini baada ya kipindi cha miezi sita kupita bei hiyo imepanda hadi kufikia dola 650 kwa tani kwa mchele wa daraja la chini uliozoeleka nchini wa ‘mapembe’.
Alisema sio lengo la Serikali kuona wananchi wake wanapata taabu, hivyo juhudi kubwa zimekuwa zikiendelea kuchukuliwa katika uzalishaji wa mchele kupitia kilimo cha Umwagiliaji maji ili kuondokana na tatizo hilo.
Alieleza kuwa moja ya juhudi hizo ni ile hatua ya Korea Kusini kusaidia kilimo cha umwagiliaji maji katika mabonde ya Zanzibar, ambapo takriban hekta 2000 zitalimwa.
Aidha alisema Serikali inaendelea na juhudi ya kutafuta uwezo na ufadhili utakaowezesha kulima hekta 6000 zilizobaki (katika mabonde ya umwagiliaji), na kuainisha kuwa hatua hiyo ikifikiwa Zanzibar itaweza kujitegemea kwa mchele kwa asilimia hamsini.
Makamu wa Rais alipingana na malalamiko ya baadhi ya wanachama hao juu ya upandaji huo wa gharama za maisha na kuwakumbusha kuwa alichoahidi katika kampeni zake za kuwania Urais ni kuwa angelifanya mambo mengi mazuri iwapo yeye angelikuwa Rais wa nchi na sio vinginevyo.
Akizungumzia hoja ya kuondolewa kwa Makontena katika eneo la Darajani, madai yanayohusishwa yanatokana na Chama hicho kumezwa katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo katika mfumo wa Umoja wa Kitaifa na amekanusha kuhusika na maamuzi ya kuyaondoa Makontena hayo kupitia Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, kama wengi wanavyodai.
Alisema yeye daima msimamo wake hauyumbi, na kurejea kauli yake kuwa eneo lolote ambalo wananchi wanapatia riziki zao, ni vyema wakatafutiwa mahala mbadala kabla ya kuhamishwa.
Akitoa mfano, alisema katika ziara zake za kukagua uharibifu wa mazingira kule Uwandani Vitongoji kisiwani Pemba na Maruhubi katika eneo ambalo wavuvi hulitumia kuanika madagaa, alikuta uharibifu mkubwa wa mazingira, lakini kwa kuthamini falsafa hiyo, alishindwa kutoa tamko la kuwahamisha mara moja wajasiariamali hao.
Aliwaeleza wanachama hao kuwa haiwezekani kwa Kiongozi alieko Serikalini kusimama hadharani na kuisema Serikali, kwani hiyo ni kinyume na maadili ya uongozi na kuonya yeyote mwenye kufanya hivyo hanabudi kuchukuliwa hatua.
Aliainisha kuwa mahala pekee na sahihi pa kusema hayo ni katika vikao vya Baraza la Mawaziri na kuainisha kuwa hilo limekuwa likifanyika.
Aliwahadharisha wanachama hao kuwa wale wanaolalamika hivyo ni watu wenye lengo la kuwafitinisha kati ya viongozi na chama chao, sambamba na kutumia fursa hiyo kuanza kuwatukana viongozi ikiwemo yeye.
Katika hatua nyingine Maalim Seif aligusia malalamiko ya wanachama wa Chama hicho ya kuwa Serikali ya awamu ya Saba ina Umoja wa kitaifa katika ngazi ya juu tu na imekuwa ikiwanaufaisha watu tisa pekee, akiwemo yeye na Mawaziri toka CUF.
Alisema hali hiyo inatokana na muongozo wa Katiba na sio vinginevyo, hatua inayompa Rais mamlaka ya kutokuingiliwa katika uteuzi wa Watendaji wakuu wa Serikali,wakiwemo Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na watendaji wengine.
Alisema katika muongozo huo wa kikatiba hakuna kipengele kinachomtaka Rais kuteua watendaji wakuu wa serikali kwa uwiano, kinyume na madai ya wanachama hao, wanaodai umoja huo ungelianzia kutoka ngazi ya shina hadi Taifa.
Vile vile Katibu Mkuu huyo, alitumia kikao hicho kuwafahamisha wanachama juu ya uwajibikaji mzuri wa Wawakilishi na wabunge kutoka Chama hicho baada ya kuwepo malalamiko kuwa wamekuwa hawatekelezi ipasavyo wajibu wao majimboni.
Alisema viongozi wa chama hicho waliokuwa ziarani kisiwani Pemba hivi karibuni, wamethibitisha kuwa viongozi hao wa kuchaguliwa na wananchi wanatoa michango yao ya hali na mali ili kuinua hali za wananchi kiuchumi na kijamii.
Alisema viongozi hao sasa wameelewa wajibu wao, ingawaje kuna baadhi bado hawajaelewa majukumu yao, na kuainisha kuwa hatokuwa tayari kupokea hoja zozote kutoka kwao kwa kushindwa kuwahudumia wananchi waliowachagua, ilhali mapato yao yanalingana na viongozi wenzao.
Hatimae Maalim alizungumzia ukimya uliotanda juu kutoonekana na kusikika kwake na kusema kuwa hiyo inatokana na udhaifu wa afya yake na kusema hali hiyo inamfanya kushiriki katika shughuli chache tu zile zilizo muhimu zaidi hadi pale hali yake itakapotengemaa vyema.
JIBU NA SWALI LAKO
10/05/2011 kwa 8:18 mu ·
mimi nauliza hawa maharamiya wameanza leo na jana si wako toka miaka hiyo na wanafanya wizi wao na hali mbaya ya znz iko pale pale hilo seif no.pia umesema kuwa hakuna kiongozi aliyejuwa ktk hawa wa cuf majukumu yao lakini sasa wanajuwa sasa kumbe sisi tuliwachanguwa wakazi ngani kama watu wenyewe hawajuwi hata wajibu wao?
pia unasema wewe sio raisi na kama watu wanataka vitu na mambo kubadilika wakuchanguwe wewe watu wakuchanguwe mara ngapi ndio ujuwe umechanguliwa maana 2010 kila moja anajuwa kama shein hakushinda wewe ndiye uliyeshinda sasa mbona akaekwa shein na wewe ukakubali kuwa makamo wa raisi na kama unajuwa kama makamo wa raisi haitowanufaisha wananchi wako basi ulikuwa huna haja ya kuingiya ktk serekali ya umoja wa kimataifa.
kisha unasema kuwa sio viongozi wote wanaonufaika na serekali ya umoja wa kimataifa na wangazi za juu tuu sasa kuna tafauti ngani kati ya serekali zilizopita na hii maana zilizopita pia ilikuwa nikujinufaisha wao tuu ngazi za juu na wewe unajuwa kama ndio hayo usingelikubali kabisa au hata sasa unaweza ukasema mimi najitowa maana sitaki wananchi wangu waone niko hapa na hakuna moja linalokuwa lakini kama wewe hapo ushafika na huku unajuwa fika kuwa wananchi wanateseka na hakuna vyakuwasaidiya sasa faida ya wewe kuwa hapo ni nini?
unasema watu wenye kuwasema nyinyi viongozi wa cuf ni wachochezi wa kutaka kuzusha fitina kati yenu na wananchi sasa hayo sindiyo waliyokuwa wakisema ccm siku zote kutudanganya kuwa watu wanakutiyeni chuki mutuchukiye kisha wao wanapanda maprodo yao wanakwenda majumbani kwao mlo mzuri sisi wanyonge tunarudi kwenye vipanda hata sio nyumba tunachemsha muhogo sasa wapi unatupeleka seif?
kama unaumwa sana na unaona huwezi tena pirika za hapa na pale basi jiuzulu watu wajuwe maana watu hawaelewi unavyosema kuwa mimi naumwa wao pia wanaumwa tena namaisha na ishakwenda zaidi ya miaka 50 na bado wanaendeleya na kumwa watu wengi sana walifikiri seif ndio mkombozi bali sasa watu washanza kukuelewa maana sio sababu ya kuwa wewe ushajuwa kuwa serekali hii haedi kama ulivyotaka na bado unaghaghaniya maana yake nini??
No comments:
Post a Comment