Saturday, May 14, 2011

SHEIN ANATAKA SEREKALI ISIHOJIWE JE YEYE NI RAISI AU DIKTETA...?

RAISi AU NI DIKTETA WA KUWAUWA WAZENJI

Ni kweli Dk. Shein anataka serikali isihojiwe?
Kalamu ya Jabir Idrissa
RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein anakwenda wapi?Ametoa kauli kuhusiana na tuhuma kuwa serikali imekodisha majengo kinyemela. Kauli yenyewe ndio imezua mgogoro.Anasema, “Serikali haifanyi makosa, ina uamuzi wake, hasa kwa mali zake, hakuna anayeweza kuihoji na ikiamua kuuza jengo itauza. Jengo lile (Mambomsiige) ni mali ya serikali. Hatujauliza mali ya mtu.“Wengine wanasema hatujatangaza tenda, kwani lazima kutangaza tenda? Mbona majengo mengine tuliyoyauza hatukutangaza tenda. Ile ni mali yetu hakuna wa kutuzuia… hili jambo serikali imeamua, sasa sioni tatizo liko wapi kwani mtu akiamua kuuza chake, nani atakuzuia? Hakuna, ni hiyari yetu.”
Alisema hivyo alipokutana na waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Ndege wa Zanzibar, akitokea ziarani nchini Uturuki, wiki iliyopita. Hajakanusha kauli hiyo iliyonukuliwa na vyombo vya habari vikiwemo vya serikali.
Nachukulia ni kauli thabiti. Ndipo ninapouliza, “Hivi rais Dk. Shein ana maana gani kusema hivyo?”
Sina shaka anajua aliapa kabla ya kuitwa rais. Pale alikuwa rais mteule. Bali alipoapishwa tu kwa kushika msahafu, aliapa kutii katiba ya Zanzibar.
Aliapa kuiongoza Zanzibar na watu wake. Aliahidi kuongoza kwa kufuata misingi ya sheria na katiba. Kwamba ataiheshimu, kuilinda na kuitetea Katiba ya Zanzibar. Na aliomba Mwenyezi Mungu amsaidie.
Sasa anaposema serikali haihojiwi kwa kuwa inauza (au kukodisha) mali yake, namuuliza amesahau kiapo hicho? Kwa asili, serikali haina mali, bali vile inavyojinasibu kuvimiliki ni mali ya wananchi.
Wananchi ndio wamiliki. Pasipokuwa na serikali, huchagua watu wao kuendesha mali hizo. Uendeshaji wake unataka uwazi na uadilifu.
Kwani, Dk. Shein hajui yeye ni rais kwa kuwa wananchi wa Zanzibar wamechoka migogoro? Kwani hajui kuwa mshindani wake mkuu katika uchaguzi, Maalim Seif Shariff Hamad, ni mvumilivu sana na mwerevu?
Ukweli, watu wamechoka kuendelea kuona nchi yao inasinzia kimaendeleo kutokana na migogoro ya kisiasa inayokua kila baada ya uchaguzi. Hii ndiyo historia.
Wamechoka, ndio maana wakachagua maridhiano. Wanataka amani ya kweli istawishwe ili wapate maendeleo kama raia na maendeleo ya nchi yao.
Hata kidogo hawajatumaini kupata rais anayejivuna. Wanataka rais anayetambua wajibu wake kwa serikali na wao. Rais anayejua matumaini ya anaowaongoza.
Sijui kama Dk. Shein anajua kuwa pamoja na Robert Mugabe kuendelea kung’ang’ania madaraka nchini Zimbabwe, baada ya miaka 20 ya kuongoza vizuri, alianza kuivuruga nchi yake? Aliwageuka Wazimbabwe.
Moja ya yaliyomsibu hata kuifikisha ilipo Zimbabwe, nchi anayojivuna sana kuipenda kuliko roho yake, ni uongozi mbaya. Umefuta hadhi ya Zimbabwe kama taifa bora kwakila kitu.
Aligeuka mtawala badala ya kiongozi ambayo maana yake hasa ni kuongoza kwa mema.
Akaanza kusakama wapinzani – kuanzia viongozi waliokuwa wanampinga mpaka raia walioamua kuchukia Chama cha ZANU-PF ambacho mwishowe alikiongoza kwa kupuuza misingi ya mantiki ya ukombozi.
Kila atizamaye vizuri, anaona alipo Mugabe; alipoifikisha nchi aliyoisaidia kupata uhuru kutoka kwa Mwingereza. Iliyopo si Zimbabwe ile iliyofahamika hadi miaka ya 1980 kama moja ya nchi chache zilizokuwa na uzalishaji mkubwa wa chakula Afrika.
Sera za Mugabe hazikuisaidia; ziliivuruga. Uchumi ukaanguka baada ya kilimo kudhoofika; viwanda vikafungwa; njaa ikaenea nchi nzima. Mamilioni ya raia wakahama nchi yao.
Hakuna anayetamani Zanzibar ifike hapo. Ingawa imedhoofika kiuchumi kutokana na uongozi mbaya, inazo nguzo za kusimamia ili istawi vizuri.
Ila hayo yanategemea sana tabia ya viongozi. Vile wanavyotumia madaraka ina umuhimu mkubwa. Zanzibar imekuwa ikihitaji viongozi wenye utashi wa kuikuza kwa kutumia hazina ya raslimali tele iliyojaaliwa.
Viongozi wanaoifaa kwa sasa lazima wawe wanaotambua na kuheshimu utu na kujenga dhamira hasa ya kuendeleza watu. Wawe werevu, weledi na wenye huruma.
Kauli ya Dk. Shein inamaanisha ameanza kusahau alichoapa na alichoahidi wananchi. Anadharau misingi ya utawala bora; sheria na utawala unaoheshimu katiba.
Pale kiongozi akisema serikali haiwezi kuhojiwa maana inauza mali yake, anamaana kuwa viongozi wanamiliki serikali; serikali ni yao na wao ndiyo serikali. Haikubaliki.
Hatwendi hivyo, maana tukishafika hapo, tumekaribisha utawala usioheshimu sheria na taratibu. Utumishi wa umma una misingi yake, sheria ni mhimili mkuu.
Dk. Shein aliwahi kuongoza wizara ya katiba na utawala bora katika awamu ya kwanza ya Amani Abeid Karume 2000 kabla ya kuteuliwa makamu wa rais wa Tanzania Julai 2001. Ninapotaja taasisi za kulinda na kusimamia dhana ya utumishi wa umma anajua.
Anajua taasisi kama Polisi, kwa ajili ya kuchunguza na kukamata mtuhumiwa; Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwa ajili ya kuchambua ushahidi na kufungua mashitaka; Mahakama kwa ajili ya kutafsiri sheria na kutoa haki panapostahili. Anajua.
Anajua Baraza la Wawakilishi (BLW) ni kwa ajili ya kutunga sheria na kuisimamia serikali katika utendaji wake wa kila siku; anajua wizara ni kwa ajili ya kuandaa na kutekeleza sera za kutolea huduma kwa jamii.
Anajua umuhimu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG); ni kuchunguza mwenendo wa matumizi ya fedha za serikali.
Hivyo ni kweli serikali isihojiwe? Basi wizara, idara na hizi taasisi za kidola tuzifute kuanzia sasa? Ndivyo? Kwamba tuziache zinunue bidhaa na kupata huduma bila ya zabuni? Na ile Sheria Na. 9 ya Manunuzi ya Huduma na Mali ya Umma ya mwaka 2005 nayo tuifute?
Basi Zanzibar tufute sheria zote; tufute polisi; tufute ofisi ya DPP, CAG, BLW na tufute mahakama. Tufute taasisi za kuchunga uadilifu na nidhamu katika utumishi wa umma na maisha ya wananchi; kweli?
Tukishafanya hivyo, tumeirudisha nchi ilivyokuwa baada ya 12 Januari, 1964. Serikali iliendeshwa kwa amri za rais – decree. Turudi huko leo? Haiwezekani.
Ni kukaribisha uongozi wa mkono wa chuma katika karne hii. Wazanzibari hawako tayari kwa hilo. Vituko vya utawala huo ndivyo walivyovichoka.
Wanataka uongozi mwema. Wanataka rais anayewapenda na kuwathamini. Anayetambua haki zao; bali pia anayejua mipaka yake kama kiongozi. Siyo kiongozi holela.
Kama Dk. Shein anajua serikali imeuza majengo ya umma, alipaswa aeleze imeuzaje. Utaratibu ulifuatwa? Wakitokea wananchi wanahoji, serikali iseme tu “tumeuza hivi na vile.”
Dk. Shein amerithi serikali. Anapokubali mema yaliyotendwa na waliopita, akubali pia mabaya yao. Haya huelezwa kwa uungwana na penye makosa wananchi huombwa radhi.
Kukubalia watu kwenda mahakamani si kurekebisha mabaya. Ni kuwatisha maana ni yeye anayeteua jaji mkuu, majaji, mahakimu, DPP, CAG.
Sasa wanaohoji ukodishaji wa Mambomsiige wakashitaki. Ni uamuzi sahihi kwani ni mahali pazuri pa kuanzia. Ni kweli huko ndiko haki hupatikana. Bali pia huko ndiko viongozi jeuri hunyooshwa.

No comments:

Post a Comment