Imeandikwa na Awadh Ali Said, Rais wa Chama Cha Wanasheria Zanzibar (Zanzibar Law Society):
Nimepitia Tamko la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar linaloeleza kuwa Tume imefuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika 25 Oct 2015. Katika Tamko hilo ametaja kifungu kimoja cha Katiba ya Zanzibar (kif 119 (10) ) na vifungu viwili vya Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar No 11ya 1984 ( kif 3(1) na 5(a.) Naomba tuvidurusu hivi vifungu tuone jee vinatoa mamlaka ya ufutaji uchaguzi/ matokeo au vinahusu mambo mengine?
Katiba kif 119(10):
“Kiwango cha mikutano ya Tume ya Uchaguzi ni Mwenyekiti au Makamo Mwenyekiti na wajumbe wanne na kila uamuzi wa Tume ni lazima uungwe mkono na Wajumbe walio wengi”
Sheria ya Uchaguzi No 11 ya 1984:
Kif 3(1) “Kanuni, maelezo na matangazo yote ambayo Tume ina mamlaka ya kutunga au kutoa , itajaaliwa kuwa yametungwa au yametolewa kisheria kama yametiwa sahihi na Mwenyekiti wa Tume au Mkurugenzi wa Uchaguzi”
Kif 5 (a):
“Tume itakuwa na majukumu ya:
a)Usimamizi mzima wa mienendo ya jumla katika uchaguzi wa Rais, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, na viongozi wa Serikali za mitaa kwa Zanzibar”.
Kifungu cha 119 (10) cha Katiba ya Zanzibar kinaelezea akidi (quorum) ya kikao cha tume. Hapo kinahusikaje na uwezo wa kufuta uchaguzi na matokeo yake?
Kifungu cha 3(1) cha sheria ya uchaguzi, kinazungmzia kuwa uchapishaji wa kanuni, maelekezo na taarifa za tume zitatolewa kwa saini ya mwenyekiti au mkurugenzi. Kinahusikanaje na uwezo wa kufuta uchaguzi wa matokeo hapo?
Kifungu cha 5(a) cha sheria kinazungumzia jukumu la tume, kuwa usimamizi wa jumla wa uchaguzi unaofanywa Zanzibar. Kinahusiana vipi na uwezo wa kufuta uchaguzi na matokeo yake?
Aibu kwa ofisi ya Mwanasheria Mkuu
Amma kweli mfa maji hukamata maji.
No comments:
Post a Comment