NI kwa sababu tu viongozi wakuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na hususan hawa wa hapa nchini Zanzibar, wamezoea kuishi kwa kuamini uongo, na kujilazimisha kutosoma alama za nyakati, wamejikuta wakisema weee, lakini wakiuficha ukweli.Mpaka sasa wanapoendelea kueneza kasumba kupitia kwa makada wao kama Humphrey Polepole, hawajakiri kuwa wameshindwa uchaguzi.Wala hawajasema kwamba yale madai wanayoyatumia kulisha kasumba wanachama na wapenzi wao pamoja na ((Watanzania)) wengine, yameshindwa mbele ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC). Yameshindwaje madai yao...?? Waliyawasilisha kwenye Tume hii ya Mwenyekiti aliyejidhalilisha na kujifedhehesha, Jecha Salim Jecha, baada ya kugundua wameshapigwa mwereka, na yote yakakutwa mazito kwa maoni yao lakini yaliyo mepesi kama usufi kwa mtizamo wa Tume na baadhi ya waangalizi wa kimataifa.Madai yao yalionekana hayana mashiko mbele ya kanuni na taratibu zinazotokana na Sheria ya Uchaguzi Na. 11 ya Mwaka 1984. Walitoa madai – hayahaya ambayo bado wanaendelea kuyatumia kuwazuga wanachama wao na watu wengine wasiojua ukweli wa kilichotokea vituoni mwa uchaguzi – wakati siwo, ingawa walisikilizwa na yakatupwa.Wanaposema mawakala wao katika vituo, ambavyo hawajapata kuvitaja, zaidi ya kueleza mambo kwa ujumlajumla tu, hawakupatiwa vitambulisho vya kutambuliwa kuwa mawakala, wanataka kusema kuwa mawakala wao walikuwa degelezi hadi kuruhusu uchaguzi kuanza bila ya wao kuwepo vituoni....?? Mimi nilishuhudia malalamiko ya Chama cha Wananchi (CUF) ya kwamba mawakala wao karibu Unguja nzima, walikuwa wanalalamika hawajapewa vitambulisho vyao kufikia magharibi ya Jumamosi, siku ya mkesha wa upigaji kura uliofanyika Oktoba 25, 2015.
Sikusikia malalamiko ya CCM popote pale. Kabla ya hapo, sikuwahi kusikia hata wakati mmoja viongozi wa CCM wakilalamikia utendaji wa Tume ya Uchaguzi. Hata mara moja sina kumbukumbu ya dhahiri.Bali ninazo barua nyingi za malalamiko ya CUF kuhusu hujuma zilizoandaliwa chini ya udhamini wa CCM kupanga njama za kuvuruga uchaguzi. Njama zilitajwa kuanzia tangu kwenye uchambuzi wa kukata upya majimbo ya uchaguzi.Ndio maana leo unalipata jimbo la Fuoni, lile ambalo lilikuwa moja ya majimbo katika Mkoa wa Mjini Magharibi yaliyokuwa na wapigakura zaidi ya 6,000 kila moja, uchaguzi huu limebaki na wapigakura 1,500 tu, idadi ambayo haikubaliki kwa mujibu wa Katiba, katika utaratibu unaoipa Tume mamlaka ya kugawa majimbo.Fuoni lilivunjwa ngaa, na pembeni yake kukapatikana majimbo mawili – Kijitoupele na Pangawe. Majimbo haya ndiyo miongoni mwa majimbo manne mapya yaliyokataliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kuwa “hawakupata nafasi ya kuyapitia na kuchambua kama vigezo vilitimia.”Ni nani kati ya CCM leo anayethubutu kusema hadharani kuwa ukataji majimbo mapya ya Zanzibar na kuyafanya sasa 54 badala ya 50, ulikuwa mpango mahsusi wa kutengeneza mazingira ambayo yataiongezea chama hicho idadi ya viti vya uhakika wakati wa uchaguzi. Hakuna atakayetoka hadharani na kusema haya kwa sababu siku zote madhalimu huwa hawayasemi waziwazi maovu wanayoyapanga, isipokuwa hukutwa tu hadharani yakitekelezwa.Safari hii, tofauti na mazoea, watekelezaji wa mpango wa CCM kujigemea viti, ambao ni ZEC, hawakutumia nguvu kubwa ya ujenzi wa hoja. Walisema tu wamefanya utafiti wa kitaalamu na walipochelewesha kutoa muundo mpya wa majimbo, walisema tu, “wala hatujachelewa.”
Umeona wapi majimbo na mipaka yake yakatangazwa siku nne kabla ya uchaguzi..?? Lakini wanasema wachambuzi wa historia ya siasa za nchi ya Zanzibar hapa kuwa lolote lisiloweza kutokea popote duniani, hutokea hapa nchini Zanzibar bila shida.CCM wanaposema kuna kura feki ziliingizwa nchini na Maalim Seif Shariff Hamad, tena hili likiwa limepigiwa chapuo na watu wasomi kama Balozi Ali Abeid Karume, achilia mbali ngumbaru kama jamaa yangu Vuai Ali Vuai, Naibu Katibu Mkuu wa CCM nchini Zanzibar, mbona hawaelezi kama walipobaini uchafu huo walipeleka ripoti kituo chochote cha polisi na uchunguzi umefanywa ikathibitika...?? Hawakufanya hivyo kwa sababu wanajua wameeneza uongo, tena katika wakati usiofaa kwani walitakiwa kusema hayo mapema kabla ya Oktoba 25, ili kura hizo zikamatwe, wahusika kuzichapisha, kuzisafirisha na kuziingiza nchini Zanzibar wakamatwe na kushitakiwa.Viongozi wa CCM, Vuai, Pandu Ameir Kificho, Shamsi Vuai Nahodha, walifika mbele ya Tume na kutoa madai haya na mengine ya kipuuzi sana. Walitupwa kwa kuwa hayafai, hayana msingi na uzushi.Ajabu, wakati wanaeneza madai hayo kwa watu wao kama mbinu ya kujikusuru (kujifariji) kutokana na dhoruba kali ya kushindwa uchaguzi iliyowaangukia, hawasemi kama wakala mkuu wa kura za urais za mgombea wao, Mohamed Ramiya Abdiwawa, alishamwaga wino kwenye fomu ya matokeo.Mimi nimekuwa nikiwauliza wananchi hapa, hivi katika mfumo tulionao ((Tanzania,)) yupo msimamizi wa uchaguzi jimboni mwenye kifua cha kuzuia kitambulisho cha wakala wa CCM...?? Au kuna jasiri gani katika viongozi wa upinzani mwenye ubavu wa kuchapisha karatasi za kura Afrika Kusini, kule zilikochapishwa zilizotumika katika uchaguzi mwaka huu, halafu akazisafirisha mpaka kuingizwa vituoni. Wote wanasema hilo haliwezekani.Lakini hili ndilo moja ya madai ya waheshimiwa sana CCM, wanaoeneza uongo ili waaminike kwamba wanahoja ya kumuunga mkono Mwenyekiti Jecha aliyefanya uhalifu mkubwa kutangaza kufuta uchaguzi siku ya mwisho aliyotakiwa kutangaza mshindi wa uchaguzi.
Viongozi hawahawa wa CCM wanashikisha propaganda watu wao kuwa Maalim Seif aliingilia mamlaka ya Tume kujitangaza mshindi wa uchaguzi. Lakini hawasemi ni kipi kilichowazuia wao ambao ndio wenye Serikali, Polisi, Usalama wa Taifa na Jeshi la Ulinzi, kuagiza akamatwe na kushitakiwa...?? Wasaidizi wa Maalim Seif wamenithibitishia kiongozi huyo mpendwa zaidi na Wazanzibari miongoni mwa wanasiasa wa nchi ya Zanzibar na Tanganyika, hajawahi kuhojiwa na mtu yeyote kijinai kuhusu tuhuma hiyo wala ile ya kuwa amechapisha kura feki na kuziingiza nchini.Hata ingekuwa amejitangaza mshindi Maalim Seif, bado Tume ilikuwa na uwezo wa kumsuta basi kwa kutangaza matokeo mpaka mwisho; kwa sababu kinyume na anavyoamini Polepole, Kifungu 12 cha Ibara ya 119 ya Katiba ya nchi ya Zanzibar, kinaelekeza:“Katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii, Tume haitalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu yeyote au Idara yoyote ya Serikali, au maoni ya chama cha siasa.”Maana yake, kama ilivyo mahakama, wakati anayeingilia mwenendo wake kuhusu kesi fulani aweza kuadhibiwa, haizuiliki kuendelea na utaratibu wake maana haifuati amri wala maagizo ya mtu yeyote. Kwanini basi Jecha akafuta uchaguzi wote wakati hana mamlaka yoyote ya kisheria...?? CCM wameumbuka na wakubali sheria na katiba, si uongo na ushetani. Kama wamefanikisha “goli la mkono” kwa uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano, kwa huu wa Zanzibar, wameshindwa. Wasalimu amri kiungwana badala ya kuhofia visasi visivyokuwepo. Kwani walifanya nini........???
No comments:
Post a Comment