Monday, July 4, 2011

GNU-YAPANDISHA BEI YA KARAFU KWA WAKULIMA ILI WAFAIDIKE


Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imepandisha bei ya zao la karafuu kwa asilimia 80 ikiwa ni sehemu ya mkakati wa miaka 10 kufufua zao hilo. Akitangaza bei mpya kwa waandishi wa habari jana katika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO), Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui,alisema “Ili kulifanya zao la karafuu na biashara yake iwanufaishe zaidi wakulima,Serikali imeamua kuanzia sasa kuwalipa wakulima wa karafuu asilimia 80 ya bei ya kuuzia katika soko la kimataifa”
Waziri Mazrui alisema katika msimu wa mwaka huu karafuu daraja la kwanza itanunuliwa na Shirika la Biashara la Taifa(ZSTC) kwa kg1 shilingi 10,000 na pishi yenye kiwango hicho itanunuliwa kwa shilingi 15,000. Karafuu daraja la pili itanunuliwa kwa kg1 shilingi 9,500 na pishi shilingi 14,250 ambapo karafuu daraja la tatu itanunuliwa kwa kg1 shilingi 9,000 wakati pishi itanunuliwa kwa shilingi 13,500.
Alisema kuanzia mwezi Januari mwaka huu,Serikali ilianza kufuatilia mwenendo wa bei ya karafuu katika masoko ya dunia kwa madhumuni ya kuandaa bei mwafaka ya kununulia karafuu kulingana na soko la duania la zao hilo. “Utafiti huo wa mwenendo wa bei katika soko la dunia ulikusudiwa pia kuiwezesha Serikali kuandaa Sera mwafaka ya bei kwa ajili ya kuendeleza zao la karafuu…Kwa hayo yote mawili, Serikali imefanikiwa vizuri sana” .
Alisema Waziri Mazrui. Waziri huyo alisema ili kutekekeleza azma ya Rais Dk Ali Mohammed Shein ya kuimarisha zao la karafuu, Serikali imeandaa na kuanza kutekeleza mkakati maalum wa kuendeleza zao hilo kwa kipindi cha miaka 10. Alisema katika utekelezaji wa mkakati huo, Serikali itajielekeza katika maeneo makubwa matatu ambayo ni kurekebisha muundo wa ZSTC kwa kubainisha majukumu yake mapya,kuweka sheria mpya kwa ajili hiyo na kuimarisha kiutendaji kwa kuajiri wafanyakazi wenye uwezo zaidi na mbinu mpya za kibiashara.
 Waziri Mazrui ameutaja mkakati wa pili ni kuimarisha mfumo na taratibu za uendeshaji wa biashara ya karafuu kimataifa ikiwa ni pamoja na kuipatia karafuu ya Zanzibar utambulisho maalim wa kimataifa ili kudhibiti magendo na uuzaji holela wa karafuu za Zanzibar. Mkakati wa mwisho umetajwa kuwa ni kuanzisha mfuko wa maendeleo ya karafuu ambao pamoja na mambo mengine, utashughulikia kilimo cha zao hilo,pamoja na kutoa huduma za kitaalam za kuendeleza karafuu

No comments:

Post a Comment