Mwakilishi wa Jimbo la Wete (CUF), Asaa Othman Hamad.
WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wameitaka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwasilisha mswaada wa sheria ya kuanzisha Shirika la maendeleo ya petroli Zanzibar kwa ajili ya kusimamia utafutaji na uchimbaji wa mafuta Visiwani Zanzibar na kutishia kuzuwia shilingi kwa bajeti ya wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati.Karibu Wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi waliochangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ardhi, Makaazi Maji na Nishati wameitaka Serikali kufanyia kazi kilio cha wananchi kuhusu kuyaondoa mafuta na gesi asilia katika orodha ya mambo ya Muungano.
Wawakilishi sasa wameibana SMZ kutoa tamko mbele ya Baraza hilo lini itawasilisha mswada wa sheria kuanzisha chombo kitakachosimamia utafutaji na uchimbaji wa mafuta wakimaanisha mbadala wa TPDC huku wakitishia kuikwamisha bajeti ya Waziri Ali Juma Shamhuna iwapo hatokuja na jibu sahihi kuhusiana na suala hilo wakati wa kujumuisha hutuba yake..
Mwakilishi wa Jimbo la Wete (CUF), Asaa Othman Hamad alisema “Tunataka iletwe sheria hapa ya kuunda chombo cha utafutaji na uchimbaji mafuta” Alisema Mwakilishi huyo.
Alisema wakati wa maneno matupu umeshapita na kinachopaswa kufanywa sasa na SMZ ni vitendo katika suala la mafuta kwa kuwa katika uchumi hakuna siasa zaidi ya siasa kutumikia uchumi.
“Tunataka siasa kutumikia uchumi, tuna haki ya kulinda uchumi wetu” Alisema na kusisitiza kwamba ndani ya Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) kuna fedha nyingi za Zanzibar ambazo haziwanufaishi Wazanzibari.
Mwakilishi huyo alisema “Mheshimiwa Spika,Mwenendo unaokwenda Serikali wallah tutakuja lizana,tena machozi ya kuku na vizazi vyetu” Alisema Mwakilishi huyo.
Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe (CUF), Ismail Jussa alisema suala la mafuta na gesi asilia limeshatolewa uamuzi na Baraza la Wawakilishi na kinachotakiwa sasa ni Serikali kutekeleza maamuzi ya Wazanzibari waliyoyafanya kupitia Baraza hilo .
Jussa alisema Serikali haipaswa kuwa na kigugumizi katika suala hilo huku akisema kwamba atazuwia shilingi katika bajeti hiyo hadi hapo atakapoambiwa lini serikali itaunda chombo cha kutoa leseni za kazi za uchimbaji wa mafuta pamoja na sheria yake kuwasilishwa katika baraza la wawakilishi kujadiliwa na wawakilishi wa wananchi kwa kuwa tayari suala hilo limeshatolewa maamuzi na kikao cha bara hilo.
“Nitazuwia shilingi katika bajeti hii hadi hapo nitakapopatiwa ufafanuzi wa kina nataka waziri atuambiye lini mswaada wa sheria utawasilishwa katika kikao hichi ujadiliwe” alihoji Jussa na kuongeza kwamba.
“Mheshimiwa Spika hili baraza ndio chombo cha maamuzi ya wananchi wa Zanzibar na baraza hili lina heshima na taratibu zake masuala yote nchi hii hayawezi kuamuliwa popote pale zaidi ya chombo hiki lakini jambo la kushanagaza suala hili la maamuzi ya wazanzibari juu ya suala zima la utafutaji na uchimbaji wa mafuta kuwa ni suala la wazanzibari wenyewe limeshatolewa maamuzi na kikao cha baraza la wawakilishi kilichopita na kwa mujibu wa kanuni za baraza jambo ambalo limeshajadiliwa na kutolewa maamuzi ni marufuku jambo hilo kujadiliwa sasa inakuwaje mheshimiwa Spika suala hili linarudi tena wakati kujadiliwa? Alihoji tena Jussa.
Jussa amesema wananchi wamechoka sasa na kauli za wanasiasa katika suala hilo kwa kuwa wanadanganywa na kuambiwa kwamba suala hilo limo katika kero za muungano kumbe wengine wakisema halimo jambo ambalo limekuwa likiwazonga na kuwababisha wananchi juu ya misimao ya viongozi wa kisiasa
Aidha Jussa amekerwa na kauli za Waziri Samuel Sitta kule bungeni na kusema kwamba zimekuwa hazina msimamo kwani waziri huyo amelidanganya bunge na kuwadanganya wananchi kuwaeleza kwamba suala la mafuta na mipaka yake.
“Waziri Sitta anatukebehi wazanzibari kutokana na uungwana wetu lakini huu uungwana kuna siku tutaukataaa, Mheshimiwa Sitta ni kigeugeu na amewadanganya wananchi na amelidangana bunge kusema kwamba suala la mafuta lipo katika mipaka aliyoitaja hizi ndizo ramani za za maeneo yanayopita mafuta” alisema Jussa huku akionesha ramani zenye michoro.
Mwakilishi wa jimbo la Kwamtipura (CCM) Hamza Hassan Juma Hamza alisema suala la mafuta na gesi ufumbuzi wake umepatikana ikiwemo azimio la baraza la wawakilishi kutaka kuondoshwa kwa suala hilo katika mambo ya orodha ya muungano.
“Sisi tunachotaka hapa ni waziri kutuambia lini sheria ya kuchimbwa mafuta na gesi italetwa katika baraza la wawakilishi kwa kuijadili na kuipitisha ili kutoa nafasi ya kazi za uchimbaji mafuta na sio jambo jengine lolote maana hivi sasa sisi wazanzibari hatutaki kusikia jambo jengine” alisema Hamza.
Hamza alisema suala la kuchimba mafuta na gesi ndiyo tegemeo kubwa la wananchi ambapo alisema haungi mkono bajeti hiyo hadi hapo atakapopatiwa ufafanuzi wa kina kwa nini serikali ipo kimya katika suala la uchimbaji wa nishati na gesi, jambo ambalo tayari limeamuliwa katika baraza la wawakilishi mwaka jana.
Akichangia mjadala huo Mwakilishi wa Jimbo la Mkwajuni (CCM) Mbarouk Wadi Mussa (Mtando) naye amesema shilingi yake ataizuwia katika bajeti ya wizara hiyo kama hatopewa maelezo ya uhakika juu ya suala la mafuta kwani hakuna hatua zaidi ya kuambiwa wazanzibari sheria hiyo itawasilishwa lini barazani.
“Mheshimiwa spika mimi kama wenzangu naungana nao kwamba nitazuwia shilingi yangu katika bajeti hii kama sijapewa maelezo ya kina na usahihi kabisa kwa nini hadi sasa serikali imeshindwa kuchimba mafuta na gesi wakati baraza la wawakilishi limeshatoa maamuzi na kwa nini mswaada haujawasilishwa ndani ya baraza hili”alihoji Mbarouk.
Mwakilishi wa Jimbo la Chaani (CCM) Ussi Jecha Simai alishangazwa hadi leo hakuna juhudi zozote za kuchimba mafuta wala gesi ambayo zipo fununu kwamba nishati hiyo ipo visiwani hapa.
Alimtaka waziri kuwaambiya wananchi wa Zanzibar lini sheria ya kuchimba mafuta na gesi itakamilika na kuwasilishwa katika chombo cha kutunga sheria yaani baraza la wawakilishi.
“Wazanzibari wanataka kujuwa lini sheria ya kuchimba mafuta na gesi itawasilishwa katika baraza la wawakilishi….jamani mafuta na gesi ndiyo mkombozi wa uchumi wetu kwa hivyo kama yapo basi ya yachimbwe ili tuweze kutatua matatizo yetu ya kiuchumi maana hata misaada hatutasumbuka kuomba tutakuwa na rasilimali yetu wenyewe iakayotunuifaisha” alisema mwakilishi huyo.
Akitoa mfano ya taifa jipya la Sudan Kusini Mwakilishi huyo alisema taifa hilo limegunduwa mafuta na gesi na wao wapo katika hatua za taratibu za kuchimba nishati hiyo ili kuondokana na umasikini mkubwa.
Mwakilishi wa Jimbo la Chonga (CUF) Abdallah Juma Abdallah alisema amepatwa na wasiwasi kwa viongozi wa Zanzibar kukaa kimya katika suala la mafuta na gesi huku baadhi ya viongozi wakiwa nje ya nchi kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kuchimba mafuta.
“Nimesikitishwa sana na ukimya mkubwa kuhusu Zanzibar katika suala la mafuta na gesi…juzi nimeona waziri mkuu Pinda yupo Korea ya kusini kukaguwa meli itakayokuja kufanya utafiti wa mafuta…..lakini viongozi wetu wa SMZ wapo kimya katika suala hili…sasa tunataka kusikia kauli yao ” alisema Abdallah.
Mwakilishi huyo ambaye yupo barazani katika kipindi cha pili alisema hivi sasa ipo hatari kubwa katika eneo la kisiwa cha Pemba huko Kigomasha ambapo ni jirani kabisa na nchi ya Kenya kuchimbwa mafuta kinyemela kwa kuwa tayari fununu za kuwa mafuta yapo karibu na Kenya zimeanza
No comments:
Post a Comment