Lula wa Ndali Mwananzela
. .
WABUNGE na Wawakilishi wanaozungumza lugha ya “kuuvunja Muungano” wanapaswa kutoka kwanza bungeni kwa kujiuzulu nafasi zao ili waendeshe kampeni ya kuvunja Muungano. Wabunge na Wawakilishi hawa hawawezi, hawapaswi na hawatakiwi kabisa kuzungumzia kuuvunja Muungano wetu wao wakiwa bado ni wabunge au wawakilishi walioapa kulinda na kuhifadhi Katiba ya Muungano na viapo vingine vya kazi zao. Ninachosema ni kuwa hili linamhusu mbunge yeyote au mwakilishi yeyote na naweza kwenda mbele kidogo, kiongozi yeyote wa Serikali aliyekula kiapo cha “kuilinda, kuitetea na kuihifadhi” Katiba ya Jamhuri ya Muungano.Tanzania ni nchi moja“Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano. Eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara na eneo lote la Tanzania Zanzibar, na ni pamoja na sehemu yake ya bahari ambayo Tanzania inapakana nayo.” Hayo ni maneno yanayofungua Katiba yetu. Si maneno yangu mimi wala si maneno ya wapinzani au wana CCM. Ni maneno ya Katiba yetu. Ndugu zangu, hakuna nchi mbili. Wabunge na Wawakilishi wameapa kulinda hili. Katiba hiyo hiyo imeenda mbele na kusema kuwa:
“Muundo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, au wa chochote kati ya vyombo vyake na uendeshaji wa shughuli zake, utatekelezwa kwa kuzingatia umoja wa Jamhuri ya Muungano na haja ya kukuza umoja wa kitaifa na kudumisha heshima ya Taifa.” Ibara ya 8:2. Kwa maneno mengine, wabunge, wawakilishi n.k hawawezi kusimama na kuzungumzia mambo ya kuvunja umoja wetu!
Sasa hawa wengine wanapozungumza kwa jazba wakati mwingine wanatoa wapi mamlaka ya kufanya hivyo? Walipoapa walidhani wanatutania. Kama waliapa kulinda Katiba hii yenye maneno haya kwa nini tusiwaone wanavunja viapo vyao wanapozungumzia kuvunja Muungano wetu?Wanakatazwa kuwa katika chama chenye sera za kuvunja Muungano. Ndugu zangu, Katiba hii ambayo viongozi hawa waliapa tena wengi wao wakishika misahafu, inasema kuwa hakuna chombo chochote cha siasa ambacho kitaandikishwa kufanya kazi nchini ambacho “kinapigania kuvunjwa kwa Jamhuri ya Muungano” Ibara 20:2b
Kila Mtanzania analazimishwa na Katiba kulinda Umoja wa Nchi yetuKatiba yetu hii ilivyo sasa haitoi nafasi kwa Mtanzania yeyote kukaa kimya wakati nchi inataka kuvunjwa na wanasiasa uchwara au kwa kisingizio chochote. Katiba inatuambia: “Kila mtu ana wajibu wa kufuata na kutii Katiba hii na sheria za Jamhuri ya Muungano. Kila mtu ana haki, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria, kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha hifadhi ya Katibana sheria za nchi.” (Ibara ya 26). Hii ina maana ya kuwa endapo tutaendelea kuwasikia wabunge au wawakilishi wanasimama na kudai kuwa“tuvunje Muungano” tunayo haki ya kuwakamata na kuwatia pingu na kuwafikisha mahakamani kwa kuvunja Katiba. Na ni wajibu na haki ya Maspika wa Bunge la Muungano na wa Baraza la Wawakilishi kuwaitia Polisi au kuwatimua kutoka “mjengoni” wabunge wanaotaka Taifa livunjwe. Haiwezekani watu waliopa kulinda na kuihifadhi Katiba yetu wawe wa kwanza kuivunja tena wakati mwingine kwa mbwembwe na madaha wakipigiwa makofi.
Na ibara ya 28:1 inaenda mbali tena zaidi na kusema pasipo utata kuwa “Kila raia ana wajibu wa kulinda, kuhifadhi na kudumisha uhuru, mamlaka, ardhi na umoja wa taifa.” Ndugu zangu, ni wajibu wa kila “raia” si hoja wa rangi, dini, kabila, mahali aliko, au hata hadhi yake katika jamii, kulinda umoja wa Taifa. Kwa maneno mengine, raia wanaokaa kimya wakati raia wengine wanatishia kuvunja umoja wa taifa wanakuwa wamekula njama ya ukimya! Kutaka kuvunja taifa ni uhaini?Naomba nipendekeze kuwa kwa uelewa wangu mdogo – na namaanisha hilo – jaribio lolote la kuivunja nchi au kujaribu kujitenga linapakana na vitendo vya uhaini. Ninachosema ni kuwa wabunge na wawakilishi wenye kuzungumza lugha ya “kuvunja Muungano” ili “kila mtu aende zake” wanakumbatiana na kubusiana na vitendo vya uhaini. Sielewi kwa nini hadi hivi sasa si Mwanasheria Mkuu au uongozi wa nchi yetu umetoa angalizo la hatari hiyo.Wanaotaka kuvunja Muungano watoke kwanza BungeniSasa, sisemi maneno haya kirahisi. Kama kweli kuna wawakilishi na wabunge ambao wanataka kweli Muungano uvunjike ili “kila mtu aende zake” basi wanachotakiwa kufanya ni kujiuzulu kwanza Ubunge na Uwakilishi, halafu waanzishe mwamko wa kuvunja Muungano. Hawawezi kuwa wamekula kiapo cha kulinda Katiba halafu wanaenda kuzungumzia kuvunja Muungano. Sheria ya Vyama vya Siasa ya 1992 pamoja na mabadiliko yake iko wazi kuwa hakuna chama cha siasa ambacho kitasajiliwa kikiwa na lengo la kuvunja Muungano. Ibara ya 8:2b inaelezea sababu mojawapo ya chama kunyimwa usajili kuwa chama hakitapewa usajili wa muda endapo “kinapigania kuvunjwa kwa Jamhuri ya Muungano”. Sasa tunajuaje chama kinapigania kuvunjwa kwa Jamhuri ya Muungano? Naomba kupendekeza kuwa ni kwa maneno ya viongozi wake wakubwa. Na hapa ninamaanisha viongozi ambao walisimamishwa na chama hicho. Ninavyosikia wabunge wa CCM na hata wa Upinzani wakizungumza “kuvunja Muungano” huku uongozi wa juu wa vyama hivyo haukemei ninaaminishwa kuwa vyama vyenyewe vinapigania kuvunjwa Muungano – kama siyo kwanini hawakani, au kuwawajibisha viongozi wao? Kuzungumzia matatizo na kero za Muungano si uhaini.Sasa nisije kuja kueleweka vibaya lazima niseme wazi kuwa sina tatizo kabisa la kifikra au kiutendaji kama wabunge wanazungumzia kutatua matatizo au wanaonyesha kukerwa na kero za muda mrefu za Muungano. Ningeshangazwa kama wabunge au wawakilishi wangekuwa kimya. Jukumu la wabunge na wawakilishi hawa ni kuweza kutafuta suluhisho la kero hizo, wazitambue na wajitahidi kuona zinaondolewa. Katika kufanya hivyo “kuvunja Muungano” si mojawapo ya mambo wanayoweza kufanya.
Kwamba Muungano wetu una matatizo, kero, migogoro na changamoto halina shaka hata kidogo. Kwamba kuna mambo yametokea ambayo yanawafanya Wazanzibari kujisikia wanabebeshwa mzigo wa “Tanganyika” na kwamba wapo wa Tanganyika wanaoona wamebebeshwa mzigo wa Zanzibari halina matatizo. Lakini je, suluhisho ni kuvunja Muungano? Muungano wa Uingereza umepitia changamoto nyingi na bado kuna hisia za kujitenga sana. Scotland miaka nenda rudi imekuwa na hisia zake kulinganisha na Wales na England. Lakini badala ya kutaka kuvunja Muungano – japo imejaribiwa sana – wamejitahidi kujaribu kuondoa kasoro na kuimarisha zaidi muungano wao. Hili ni kweli kwa Marekani vile vile. Jimbo la Texas liliwahi kuwa nchi huru. Ni jimbo la pili kubwa zaidi Marekani (kwa jiografia na idadi ya watu) likiwa na historia yake tofauti sana na majimbo mengine. Lilipata uhuru wake kutoka Mexico na kwa muda lilikuwa ni nchi huru. Muda mrefu kuliko Zanzibar ilivyokuwa huru kutoka kwa Uingereza! Lakini, Texas ingeweza kudumu kuwa huru lakini changamoto za wakati ule na siasa za ndani zikalazimisha hatimaye Texas kujiunga Shirikisho la Marekani na kuwa jimbo la 28 kujiunga chini ya Marekani. Kujiunga kwake haina maana kuliondoa matatizo na kero mbalimbali za mahusiano ndani ya Muungano, wakati mwingine hata kauli za kutaka kujitenga tena. Ukifikiria sana, sasa hivi Texas ina uwezo mkubwa wa kiuchumi na kimaisha kuweza kuwa nchi huru kuliko miaka zaidi ya 100 iliyopita. California nayo iliwahi kuwa Jamhuri iliyodumu kwa siku 22 tu kabla ya kuvamiwa na Marekani na baadaye kuwa jimbo la Marekani. Leo hii California kiuchumi peke yake iko nyuma ya nchi saba tu zilizoendelea na hivyo kama ingetaka kuwa taifa huru ingeweza kabisa!
Lakini Texas na California pamoja na utajiri wao na matatizo yao ya kihistoria wamebakia ndani ya Muungano wa Marekani. Hawazungumzii kujitenga; hawazungumzii kuvunja muungano kwa sababu ya “kero, matatizo na changamoto”.Watoke kwanza, wabadili katiba ndipo wazungumzie kuvunja Muungano
Ni kwa sababu hiyo basi, ni lazima tutambue kuwa matatizo na kero tunazoziona kati ya Zanzibar na Tanganyika ni nafasi ya kuboresha Muungano zaidi na si kuuvunja! Ni lazima tutambue kuwa maneno “ya kujitenga” ambayo mengi yanatokana na hisia zilizoumizwa ni ya kuyakataa kwa sababu Mwalimu Julius Nyerere alisema vizuri sana huko nyuma. Tukishaanza kujitenga hatutaacha. Tukishawatenga Wazanzibari tutagundua kuwa hakuna watu wanaoitwa “Watanganyika” wapo Wachagga, Wakwere na Wasukuma. Kule Zanzibar wakishatoka kwenye Muungano na kuwavua “Watanganyika” kama koti linalowabana watajikuta hakuna kweli “Wazanzibari” bali wapo “Washirazi, Waarabu, Wanyamwezi na watu wa “bara”. Watajaribu kusema kuwa “sisi ni wamoja” lakini ukweli ni kuwa walikuwa wamoja waliposhikana na “Tanganyika”!
Ndugu zangu, wanasiasa wenye sera za kuvunja Muungano kwa kisingizio cha haki ya “kutoa maoni” wafanye hivyo nje ya Bunge na Baraza la Wawakilishi na nje ya viapo vyao. Hawawezi kuwa wameapa kulinda Muungano tena kwa kushika misahafu halafu wazungumzie kuvunja Muungano. Haiwezekani mtu wa familia moja aseme “mimi ni mwana familia” halafu asimame na dumu la petroli na kijiti akitaka kuwasha moto nyumba kwa kisingizio ati “baba hanipendi”! Watoto wengine ni lazima wasimame dhidi ya mwanafamilia huyo.Spika Anne Makinda na Spika Pandu Ameir Kificho wana jukumu pamoja na viongozi wa Serikali kwenye vyombo hivyo kusimamia Katiba ya Muungano. Wasikubali kutoa nafasi za hotuba za kuvunja Muungano kwani wawahoji hao wabunge na wawakilishi kama vyama vyao vimewatuma kutoa kauli hizo na kama ni kauli zao kwanini zisichukuliwe ni kuvunja Katiba walizoapa kulinda na kuwapa pendekezo kuwa kama wapo wanaotaka Muungano uvunjwe wajivue uwakilishi wao kwanza na waje huku mitaani kuanzisha harakati za kuvunja Muungano. Bunge na Baraza la Wawakilishi visitumike kueneza kampenzi za uhaini wa wazi na uvunjaji mkubwa wa katiba.Vinginevyo, Kificho na Makinda, Jakaya Kikwete na Ali Mohammed Shein, Mizengo Pinda na Balozi Seif Idi watakuwa wamekula njama ya kuvunja Muungano. Maana wanaonekana wamepoteza uwezo wa kutetea Katiba (waliyoapa kuilinda, na kuitetea) na zaidi wao wenyewe wametoa jukwaa kwa wanasiasa kuendesha siasa za kuvunja Muungano huku wakijua fika kuwa Katiba na Sheria walizoapa kuzilinda vinakataza. Ni kutokana na hayo nimejipa wajibu chini ya Ibara 26 ya Katiba ya Muungano kuwatuhumu wao na wale wote wenye kueneza sera za kuvunja Muungano kuwa wamekula njama ya kuvunja Katiba na hivyo kupoteza haki ya kuwa viongozi wetu halali.
Kama wanataka kuvunja Muungano kwa kisingizio au sababu yoyote ile, wajivue nafasi zao walizo nazo sasa na waanze kampeni ya kuvunja Muungano chini ya kivuli cha mwamko wa Katiba Mpya.
Lakini kwanza wafute vifungu vya Katiba vilivyo sasa ili viwaruhusu hata kutoa lugha za kuvunja Muungano kwani ilivyo sasa hata huku nje hatuna uwezo wa kuzungumzia kuvunja Muungano bila kuonekana tumekumbatiana na kubusiana na uhaini.
WEWE ULIYE ANDIKA MAADA HII NI MOJA KTK HAO WALIVI WALIOKUWEKO NDANI YA BUNGU KWA KUJALI MASLAHI YAO NDIO MAANA WANALINDA MUUNGANO HIZO IBARA ZAKO NA KATIBA KWANZA HIYO KATIBA KAMA WEWE HUJUWI SIO KATIBA YA MUUNGANO HAKUNA KATIBA YA MUUNGANO HII NI MOJA KUWA WATU WANAHAKI YA KUVUNJA MUUNGANO PILI MZEE KARUME HAKUWA RAISI Z;BAR MAANA HAKUCHANGULIWA NA WANANCHI SASA TAYARI HAPO NI HARAMU ISHAINGIA KTK MUUNGANO PIA ALIPO UNGANA NA NYINYI WATANGANYIKA HAKUWASHAURI BARAZA LA MAWAZIRI NI YEYE TU ALIJIPELEKA NA KUUNGANA NA ALIPOWAMBIA WALICHUKIZWA NDIO HAKUJA TENA DAR HATA SHEREHE YA KUCHANGANYA MCHANGA HAKUWEPO SASA MUUNGANO HUO HALALI YAKE IKO WAPI..?VIONGOZI KUAPA NI LAZIMA ILA KAMA MAMBO HAYAENDI KAMA YALIVYO KUSUDIWA BASI HATA M/MUNGU ANAWASAMEHE MAANA ANAJUWA WANAJARIBU KUTETEA HAKI SIO THULMA MAANA Z;BAR IMETHULUMIWA NA NYINYI WATANGANYIKA KWA MIAKA 47 SASA ILA HUU NDIO MWISHO WENU MUTAKI MUSITAKI WALA USILETE VITISHO HAPA KAA ULE UGALI WAKO NA KAMBARE WATU KAMA NYINYI NDIO NYERERE ALIWABATIZA NA NDIO MAANA HAMUNA FIKRA NYENGINE YA KUJENGA AMANI NA MAENDELEYO FIKRA ZENU NI KUKANDAMIZA BASI UDIKTETA KAA UNGALIYE SHOW.
No comments:
Post a Comment