Friday, July 8, 2011

POROJO LA WABUNGE NCHINI TANGANYIKA DODOMA

MAMBO NDIO KAMA HAYA KWELI WATAKUWA NA AKILI ZA KUJENGA NCHI AU AKILI ZAO ZIME JAA UBATHIRIFU NA KUNYANYASA WANANCHI.

WABUNGE wamesema matatizo ya Muungano yatamalizwa na Katiba mpya inayotarajiwa kuandikwa upya hivi karibuni.
Aidha, wabunge wa Zanzibar wamesema bado wanautaka Muungano uliopo baina ya Tanganyika na Zanzibar na kutaka matatizo yaliyopo yatatuliwe ikiwemo kuongezwa kwa idadi ya mabalozi wanaotokea Zanzibar wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi.
Walikuwa wakichangia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kwa mwaka wa fedha 2011/2012 iliyowasilishwa juzi bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan.
Hata hivyo, wabunge hao walionesha kutofautiana juu ya Serikali za Muungano huo ambapo wapo wanaotaka serikali tatu na wengine wakitaka ziendelee Serikali mbili.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) alisema matatizo ya Muungano yatamalizwa na Katiba mpya ambayo mchakato wake umeshaanza.
“Kama kweli Serikali ina dhamira kushughulikia kero za Muungano, itatoa kauli rasmi ya Muswada wa Katiba uletwe bungeni na sisi tunataka ukamilike haraka sio kusema 2014,” alisema Mnyika.
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), mbali ya kuukosoa Muungano akidai ulifanywa kwa siri na kupelekwa haraka bila wananchi kushirikishwa, suluhisho lake ni Katiba mpya.
“Kuna maswali yanatakiwa kuulizwa, je, Muungano huu wananchi wa Bara na Visiwani wanautaka; Katiba ya Muungano iwe ya ridhaa ya wananchi na je Muungano wa aina gani wanautaka?
Lakini suluhisho la matatizo yote ya Muungano ni Katiba mpya itakayowashirikisha wananchi,” alisema Lissu.
Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa (CUF), alisema kero za Muungano zilizopo sasa ni matokeo ya Katiba ya sasa.
Licha ya kuutaka Muungano huo waliodai umesaidia maendeleo na usalama kwa Zanzibar, wabunge kutoka Zanzibar waliochangia makadirio hayo walitaka kuwepo uwiano wa nafasi
za ubalozi na kiwango cha asilimia cha fedha kinachotengwa kwa elimu ya juu.
Pia walitaka kuongezwa kwa asilimia ya fedha ya mapato wanayopewa Zanzibar kutoka Benki Kuu na kuwepo uwazi juu ya suluhu inayopatikana kutokana na majadiliano ya kutatua kero
inayofanywa na Tume ya pamoja ya kutatua kero hizo.
Mbunge wa Kiembesamaki, Warde Bakari Jabu (CCM) alisema, “Muungano tunautaka na udumu, lakini matatizo yake yatatuliwe kama nafasi za ubalozi tupewe, tujue asilimia ngapi ya elimu ya juu inatengewa Zanzibar na tatizo la mikopo ya elimu ya juu litatuliwe”.
Alisema tatizo la Muungano kwa sasa ni kutokuwepo uwazi kwa mambo ya ndani
yanayojadiliwa kuhusu Muungano huo na kutaka viongozi wanapojadili kero hizo kutofanya siri na kuwaeleza wananchi kila kitu.
Naye Mbunge wa Mgogoni, Kombo Khamis Kombo (CUF) alisema suluhu pekee ya matatizo ya Muungano ni kuwepo Serikali tatu, ambapo alisema ana uhakika wakati wa kuandaliwa Katiba mpya, wananchi wa Zanzibar na Tanzania Bara wataunga mkono kuwepo Serikali hizo
tatu.
Hata hivyo, Mbunge wa Donge, Sadifa Juma Khamis (CCM) alipinga Serikali tatu akisema itaongeza gharama na kuongeza “kwa sababu ya Muungano, Zanzibar leo kuna amani na usalama nina hakika tungekuwa wenyewe kusingekuwa na amani hii.”
Mbunge wa Dole, Sylvester Mabumba (CCM) alisema kutokana na Muungano, hata yeye mwenye asili ya Tanzania Bara amekuwa Mbunge na kusema Serikali tatu hazitasaidia Muungano kwani hakuna nchi zilizoungana zikawa na Serikali tatu zikadumu, bali zote zilisambaratika.
Mbali na kutaka Muungano uwepo, alisema kuna haja ya kutatuliwa kero zake kama katika ngazi za utendaji kwenye Serikali ya Muungano Wazanzibari wapewe nafasi kama watendaji kwenye Wizara ya Elimu ya Juu na nafasi za ubalozi wa Tanzania kuwe na uwiano

No comments:

Post a Comment