Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu amemtaka Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Peter Pinda, kuwaaacha wazanzibari kutoa maoni yao kwa hisia wanazozitaka na wasikatazwe kwani kufanya hivyo ni kutoa kilio chao cha muda mrefu dhidi ya ukandamizaji wanaofanyiwa wazanzibari na serikali ya MUUNGANO.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu amemtaka Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Peter Pinda, kuwaaacha wazanzibari kutoa hisia zao kwa mustakabali wa nchi yao na kuacha kutoa
vitisho dhidi yao visivyo na lazima.
Akihutubia mkutano wa hadhara wa Chama chake uliofanyika Kibanda Maiti Mjini Zanzibar, Jussa amesema haoni mantiki ya wazanzibari kuonekana wakorofi wakati wanajadili mambo ya msingi ambapo Zanzibar ni mshirika sawa katika Muungano.
Jussa ameweka wazi kwamba hatua ya wazanzibari kuzungumzia masuala yanayohusu Muungano kwa kile kinachodaiwa ‘jazba na hamasa’ sio dhambi kwani wanafanya hivyo kwa lengo la kuitetea maslahi ya nchi yao na kinachotakiwa ni hoja za msingi ambazo wazanzibari wamekuwa wakizitoa.
“Hamasa katika kutetea haki ni sawa na sio dhambi, hasa katika jambo la kulinda
mipaka ya nchi, na hili linajulikana na yeye Pinda anajua na kama hajui basi aje Zanzibar kujifunza historia ya Zanzibar kwa sababu haijui inavyoonesha,” alisema Jussa huku akishangiriwa nawafuasi na wananchi waliofurika katika uwanja huo.
Katika mkutano huo uliokuwa na lengo la kuzindua Kampeni ya Chama cha CUF iliyopewa jina la Zinduka awamu ya Pili Zanzibar, ambapo mbali ya kuzungumzia kero za Muungano alitumia mkutano huo kuelezea mkakati wa namna ya kutoa maoni katika mchakato wa katiba mpya.
Jussa alisema anaamini katika suala kutetea haki ya Zanzibar, wananchi wote watakuwa na mshikamano wa hali ya juu kama ilivyooneshwa na wabunge na wawakilishi wao bila ya kujali vyama vyao wameonesha msimamo wa kuitetea nchi yao, hivyo hatua yoyote ya
kuwatisha ni kupoteza muda.
“Tutatetea haki ya Zanzibar hadi mwisho wa nguvu zetu, tunataka kuwarithisha vizazi vyetu
Zanzibar yenye hadhi yake, Zanzibar yenye heshima na Zanzibar yenye Baraka na amani kama ambayo sisi tumeikuta kwa wazee wetu na hatua yoyote ya kutaka kutuziba midomo haitafanikiwa kwani wakati wa kuwafunga midomo wazanzibari umekwisha,” alisema Mwakilishi huyo wa Mji Mkongwe mwenye mvuto mkubwa kwa vijana.
Wiki iliyopita, akitoa majumuisho ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi yake, Waziri Pinda alionekana kuwa mkali na kuwashutumu Wazanzibari wanatumia jazba na hamasa wakati wanapojadili masuala ya MUUNGANO.
Kwa matamshi hayo, Jussa ameuambia umati uliosheheni katika mkutano huo kuwa Wazanzibari wameipokea kauli ya Pinda kwa mshtuko na masikitiko makubwa, huku wakijiuliza katika karne hii kuwepo mtu wa kuwatisha pale wanapotetea maslahi yao.
“Tutahakikisha maslahi ya Zanzibar yanalindwa, tunasema bila ya woga bila ya khofu kwamba tunataka kuhakikisha maslahi yetu yanalindwa ….vinginevyo tutaukataa,… kwa jazba.” Alisema na hushangiriwa na wananchi waliokuwepo mkutanoni hapo.
Suala la mchakato wa katiba mpya limekuwa likijadiliwa katika makongamano mbali mbali ambapo hivi juzi wananchi wa Zanzibar walisema licha ya kuwa wameisikia kauli ya Pinda lakini hawaitaisikiliza kwa kuwa lengo ni kutoa maoni ya juu ya katiba na mustakabali wa chi yao.
Wakizungumza katika mkutano uliofanyika bwawani Azzan Khalid Hamdan alisema wazanzibari wataendelea kutoa maoni yao juu ya katiba hii na hakuna kitu ambacho kitazuwia kwani wamechukua ahadi ya kuwaelimisha wananchi juu ya suala zima la mustakabali wa nchi yao .
“Tumemsikia Pinda akisema kwamba tusipotoshe wananchi lakini sisi tunamwambia hawezi kutuziwia kwa sababu tulichukua ahadi pale bwawani siku aliyokuja kamati ya Samuel Sitta kwamba tutawaelimisha wananchi hadi wafahamu sasa kama yeye atakata kawa watu wasitoe elimu basi awakataze huko TANGANYIKA sio sisi” alisema Khalid.
Mbali na Waziri Pinda kwa upande wa Zanzibar pia Makamu wa pili wa rais
Balozi Seif Ali Iddi wakati akifanya majumuisho ya bajeti yake aliwataka wajumbe wa baraza la wawakilishi na wananchi kwa ujumla kutokuwa na jazba wakati wa kutoa maoni katika mchakato wa katiba kwa kuwa kufanya hivyo kutaifanya serikali ya MUUNGANO. kutowaelewa wazanzibari.
Aidha Jussa alionekana kumgusa makamu wa pili bila ya kumtaja jina kwa kusema kwamba yeyote atakayewagusa au kuwakataza wananchi wasitoa maoni yao kwa uwazi, watapambana na umma wa wazanzibari ambao kwa sasa hautaki tena kuendeshwa na kuamuliwa katika maamuzi yao.
Aidha Jussa aligusia suala la Mali asili za Taifa, na kusema Tanzania Bara imekuwa ikichimba madini ya aina mbali mbali pamoja na gesi mambo yanayoelezwa kuwa sio ya MUUNGANO, na kuhoji mantiki ya suala la Mafuta yanayoaminika kuwepo Zanzibar kuwa ni ya MUUNGANO.
Alimkumbusha Waziri Mkuu kuwa Hayati
Mwalimu Julius Nyerere alikuja Zanzibar na itikadi ya kisiasa na kukubaliana na hayati
Abeid Karume kuunganisha NCHI MBILI, hivyo kila upande una
haki na sababu za kuhoji yaliomo ndani ya MUUNGANO huo.
Mwalimu Nyerere alipokuja hapa Zanzibar hakuja kama padri wala hakuja kama sheikh alikuja kama mwanasiasa kwa hivyo walichokubaliana kinaweza
kubadilishwa wakati wowote” alisema Jussa.
Akizungumza katika mkutano huo Maalim Seif Shariff Hamad, Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) amewahakikishia wananchi kwamba watapewa nafasi ya stahiki wakati wa mchakato wa katiba mpya ya Tanzania.
Maalim Seif amewataka wazanzibari kujiandaa vyema na kujitokeza kwa wingi wakati ukifika kutoa maoni yao juu ya Katiba mpya wanayoitaka huku akiamini kwamba uamuzi wowote utakaofikiwa na wazanzibari wenyewe, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ilio katika mfumo wa Umoja wa Kitaifa, itaheshimu chochote kile kitakachoamuliwa na wananchi kwa kuwa Dk Shein ni rais anayeheshimu utawala wa sheria na kuwapenda wananchi wake.
BASI KAMA ANAHESHIMU NA ANAWAPENDA WANANCHI NA AVUNJE MUUNGANO KWANZA NA TUWE NA SEREKALI YETU KAMILI NA KILA KITU KISHA BAADA YA MIAKA MITANO AU KUMI NDIO ATULIZE TENA TUNATAKA MUUNGANO AU LAA KWA SASA NI LAA HAKUNA CHA MUUNGANO HATUTAKI HATUTAKI HATUTAKI.
No comments:
Post a Comment