Monday, July 18, 2011

ZANZIBAR NA GHANA KUFUFUWA URAFIKI WAO WA ZAMA ZILE

Maalim Seif Sharif Hamad akipokea zawadi kutoka kwamsaidizi wa Mfalme wa Ashanti, Otumfuo Osei Tutu, baada ya kumaliza mazungumzo yao,ofisini kwake Migombani.
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, ameiomba Ghana kupanua wigo wa ushirikiano kati yake na Zanzibar, na kuangalia uwezekano wa kuisaidia katika uimarishaji wa kiwango cha elimu.Maalim Seif ametoa wito huo leo Ofisini kwake Migombani, alipozungumza na Mfalme wa Ashanti, Otumfuo Osei Tutu.Maalim Seif amesema ushirikiano kati ya nchi mbili hizo ni wa muda mrefu, tangu wakati ule viongozi wa nchi hizo Hayati Abeid Karume, Mwalimu Nyerere na Kwame Nkrumah wakipigania Uhuru wa nchi zao na Afrika kwa jumla.Alisema katika kuendeleza ushirikiano huo, kuna umuhimu mkubwa kwa Ghana ambayo imefikia maendeleo makubwa, kuisaidia Zanzibar katika kuinua kiwango cha elimu maskulini.Alisema mbali na mipango madhubuti ya Serikali ya kuinua kiwango cha elimu ya msingi kupitia Teknolojia ya habari, Zanzibar inakabiliwa na changamoto kubwa ya upungufu wa walimu wa Sayansi kwa shule za SekondariAlieleza kuwa hali hiyo inatokana na wanafunzi wengi waingiapo Sekondari kujikita katika masomo ya sanaa (art).Aliitaka Ghana ambayo imepiga hatua kubwa katika sekta ya Elimu kuangalia uwezekano wa kubadilishana uzoefu kwa walimu wake kuja Zanzibar kufundisha, ili kuimarisha fani ya sayansi.Aidha alimuomba Mfalme huyo kuwashajiisha wawekezaji wa Ghana kuja kuwekeza katika sekta ya uvuvi wa bahari kuu, kwa maelezo kuwa kuna rasilimali nyingi ambazo bado hazijatumika ipasavyo.Alisema uvuvi unaofanyika hivi sasa ni wa kienyeji, ambapo wavuvi huvua katika maeneo ya pwani, kutokana na ukosefu wa utaalamu na kuwa na vifaa duni vya kuvulia.
Vile vile Maalim Seif alitumia fursa hiyo kumuomba Mfalme Tutu kuangalia uwezekano wa kuisaidia Zanzibar katika dhamira zake za kuimarisha huduma bora za afya, akielezea changamoto kadhaa zinazoikabili sekta hiyo, ikiwemo upungufu wa madaktari, vifaa na wataalamu mbali mbali.Maeneo mengine ambayo Maalim Seif aliomba kuendelezwa ushirikiano kati ya nchi mbili hizo ni pamoja na uimarishaji wa kilimo,hususan cha matunda na mbogamboga, akieleza azma ya wakulima wa Zanzibar kupata fursa ya kujifunza kutoka kwa ndugu zao wa Ghana.Pia Maalim Seif alimweleza Mfalme huyo dhamira ya Serikali ya Zanzibar katika kuimarisha zao la Karafuu ili kuleta ushindani na nchi kadhaa Duniani zinazozalisha zao hilo.
Alisema mbali na kuwepo uzalishaji mkubwa wa zao hilo kutoka nchi za Brazil, Indonesia,Syrilanka na Madagascar, Serikali imejipanga vyema kuirejeshea hadhi yake Zanzibar kama nchi inayoongoza kwa uzalishaji wa karafuu yenye ‘kiwango bora’ Duniani.Alisema ili kufikia azma hiyo kuna umuhimu kwa Ghana kusaidia katika utafiti.Katika hatua nyingine Maalim Seif ameiomba Ghana kusaidia utatuzi wa changamoto ya ugonjwa wa Ukimwi ili kupunguza/kuzuia maambukizo mapya sambamba na kukabiliana na uingiaji na matumizi ya madawa ya kulevya, ikizingatiwa mazingira ya Zanzibar kuwa ni ya kisiwa.Mapema Mfalme Tutu alisema Ghana na hususan Jimbo la Ashanti litaendeleza mashirikiano yake na Zanzibar kwa faida ya wananchi wake, na kuainisha kuwa taratibu za kubadilishana uzoefu zinasaidia katika kukuza maendeleo.
Aliipongeza mageuzi ya kisiasa yaliofanyika Zanzibar na kupelekea kuundwa kwa Serikali yenye mfumo wa umoja wa Kitaifa, na kusema hatua hiyo ni upanuzi wa Demokrasia.Aidha alitoa wito kwa Mataifa ya Afrika kukaa na kumaliza matataizo yao wenyewe bila ya ‘kuwaita watu weupe’ kuja kuwatatulia.

No comments:

Post a Comment