MBUNGE wa Singida Mashariki,Tundu Lissu (Chadema), ameishukia Wizara ya Muuungano na kuitaka itoe majibu ya kweli badala ya porojo kuwa Muungano ni mzuri.
Lissu alisema hatua hiyo inatokana na ukweli kuwa Muungano ulizaliwa katika mazungumzo ya siri na utata mkubwa kutokana na shirikizo la Tanganyika kuhofia kuingia katika vita baridi kutoka kwa Mataifa makubwa duniani.
Akichangia hotuba ya makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano katika mwaka wa fedha wa 2011/12, Lissu alisema haiwezekani suala la Muungano kuwa siri kwa sasa na kwamba kama kutakuwa na usiri wakati utafika wananchi watakosa uvumilivu kwani wengi wanahisi kuwa wanaburuzwa.
Maswali aliyotaka yajibiwe ni pamoja kama Wananchi wanaukubali Muungano nakama wanaukubali ni Muungano wa aina gani uwepo.
“Nasema rejeeni waraka wa Abood Jumbe Mwinyi kuhusu Muungano, unasemekana wazi kuwa Hayati Mwalimu Nyerere alimshinikiza Karume ili asaini hati ya Muungano lakini bila ya kuwashirikisha watu wengine alisema wazi yule mzee. Hii ni hatari kubwa tena hatari hii iko mbele yetu na kwa vizazi vyetu, tunahitaji kurejea hayo makabati yafunguliwe ili tuone nini kilizungumzwa,” alihoji Lissu.
Akizungumza kwa hisia kali Mnadhimu Mkuu huyo wa kambi ya upinzani bungeni, alisema kuwa haiwezekani kwa akili ya kawaida nchi mbili kuungana wakati mojawapo ilikuwa na siku mia moja tangu izaliwe jambo linaloonyesha kuwa ilikuwa changa na haikuwa imejitafakari.
“Tukihoji juu ya Muungano mnasema kuwa tunamtukana Nyerere, hii ni ajabu sana kwa nchi hii, lakini sote ni ndugu tumeungana kwa nia njema isipokuwa hata ndoa huwa zinavunjika,”alisema Lissu.
Alifafanua kuwa suala la kuukubali Muungano liliingizwa bungeni kwa hati ya dharura Juni 10 mwaka 1965 katika kikao cha 17 cha Bunge na aliyekuwa Waziri Mkuu, Rashid Kawawa na kwamba baadhi ya wabunge waliotaka kuhoji juu ya Muungano huo walinyamazishwa kutokana na misimamo ya viongozi waliokuwapo madarakani.Kwa upande wake Mbunge wa Mkanyageni Habib Mnyaa (CUF), alisema kwa hali ilivyo, serikali inalazimisha Muungano wakati ikijua kuwa kuna matatizo makubwa ambayo yanafanya sura nzima ya Muungano isionekane.
Hata hivyo mbunge huyo alihoji kama Muungano ni halali na kwamba picha ya Karume iko wapi wakati wa kuchanganya udongo Aprili 26 mwaka 1964.
Mnyaa alisema kuwa serikali imekuwa ikiwachangaya wananchi kusema kuwa kuna kero za Muungano bila ya kujua wananchi walishagundua kuwa hiyo ni danganya toto kwani kilichopo si kero za Muungano bali ni matatizo ya Muungano.
No comments:
Post a Comment